The Chant of Savant

Tuesday 2 September 2008

Pinda, usanii, EPA na kutafuta ng’ombe mfukoni



Kuna kisa kimoja cha mchungaji mwizi mpumbavu. Huyu bwana alipewa ng’ombe na mwenyewe akamchunge. Yeye aliamua kumuuza. Aliporudi kwa mwenye ng’ombe mikono mitupu aliulizwa alipokuwa ng’ombe tena dume. Alianza kujipekua mifukoni ili aone kama ng’ombe yumo.
Baada ya mwenye ng’ombe kubaini upumbavu huu wa kizamani alimuuliza, si angekuwamo angelia? Mpumbavu hakujibu baada ya kugundua kuwa utoto wake umegundulika.
Hiki kisa kinanikumbusha matukio mawili hata matatu ya kusikitisha na kuudhi. Haya tofauti na kisa chetu yametokea na kila mmoja wetu shahidi.
Tukio la kwanza ambalo nimeishalijadili ni kwa rais Jakaya Kikwete kuwasamehe wezi wa EPA. Sababu? Anazijua mwenyewe? Swali, je rais anafanya hivi kwa faida ya nani? Je hii siyo kuthibitisha ukweli kuwa naye ni fisadi kama alivyotajwa kwenye list of shame. Bahati mbaya kwake, hakujibu hoja za waliomtuhumu. Je ni kwanini? Jibu unalo msomaji mpendwa.
Suala la pili ni usanii au tuseme kitendawili cha serikali kusema itawachunguza Bangusilo Ibrahim Msabaha na Nazir Karamagi, mawaziri wa zamani waliotimuliwa baada ya kugundua kuwa waliingiza taifa hasara kwa kula njama na kampuni vidhabi za Richmond na Dowans.
Kinachokera hata kama ni kichekesho ni kumuacha nje mhusika mkuu waziri mkuu wa zamani aliyetimuliwa na Kamati teule ya Bunge, Edward Lowassa. Ni tusi na kituko kwa umma kutomhusisha mtuhumiwa na mchezaji mkuu wa kashfa hii. Kisichoeleweka zaidi ni ile hali ya Lowassa kuendelea kufaidi marupurupu na mapato ya usataafu kana kwamba alistaafu.
Rais Kikwete kipenzi na mshirika mkuu wa Lowassa, kama kawaida yake, hataki kutoa ufafanuzi wala mwelekeo wa serikali yake kuhusiana na Lowassa. Ni sababu gani zilizofanya serikali kuwachunguza mawaziri ambao kimsingi walikuwa makuadi wa Lowassa na wenzake?
Waziri mkuu Mizengo Pinda aliliambia bunge kuwa Karamagi na Msabaha watachunguzwa eti kuona kama walitenda kosa wakati ukweli uko wazi kuwa walitenda kosa. Kama hawakutenda kosa ni kwanini walijiuzulu uwaziri? Je hapa kinachotafutwa ni kama wamekosa au kutaka kuona ni jinsi gani wataonekana hawakukosa? Je huu siyo usanii mwingine wa kutaka kutuhadaa ili kuwaokoa watuhumiwa? Kwanini serikali ianzishe uchunguzi mwingine ilhali Kamati teule ya Bunge iliishachunguza na kutoa mapendekezo? Kama serikali tunayoiita yetu ingekuwa yetu basi ingefanya kitu kimoja; kuwafikisha wahusika wote mahakamani ili haki itendeke.
Nani ataiamini tena serikali ambayo ni mtuhumiwa mkuu bila kusahau chama kinachoiunda? Je watanzania wataendelea kuwa kichwa cha mwendawazimu walevi kujifunzia kunyoa? Hadi lini upuuzi huu?
Tukio la tatu ni kwa waziri wa nishati na madini, William Ngeleja kuendelea kupatwa kigugumizi kuwataja wamilki wa machimbo ya makaa ya mawe ya Kiwira yanayodaiwa kutwaliwa kinyume cha sheria na rais mstaafu, Benjamin Mkapa na washirika wake. Je watu wa namna hii ni wa kuwaamini kuendelea kukaa kwenye ofisi zetu? Hapa ndipo haja ya kufikiria impeachment inakuwa bidhaa adimu na aghali. Je watanzania wataendelea kuchezewa mahepe kweupe nao wakishangilia kiama chao? Ngeleja tafadhali tutajie wamilki wa Kiwira kama ulivyoahidi.
Kisa cha mwisho ni ile hali ya rais Kikwete kutimkia Marekani huku akiacha nchi inawaka moto kuhusiana na kadhia za muungano na kashfa za ujambazi kwenye taasisi zetu. Je huyu kweli anao uchungu na nchi? Je jeuri na kutojali huku hadi lini? Je watanzania wanaogopa nini kuamua kuirejesha hatima na nchi yao mikononi mwao?
Je hapa ni nani wa kulaumiwa?
Tumalize kwa swali kuu kwa Kikwete na watanzania wote ili kutia msisitizo kwenye usanii na ujambazi wa EPA na Richmond.

Kikwete aliwasamehe na kuwakingia kifua mafisadi kwa kisingizio cha haki za binadamu. Fine. Kwanini binadamu wawe mafisadi kiasi cha kuhujumu haki za umma wa watanzania karibu milioni 40 uliomchagua na unaolipia maisha yake ya kifalme? Hata hiyo sheria husema wengi wape. Je hawa watanzania wanaodhulumiwa haki zao kwa kisingizio cha madaraka wao siyo binadamu wanaposwa kulindwa haki zao za binadamu? Je nani walimpa ushindi wa kishindo cha Tsunami Kikwete kati ya wananchi na mafisadi? Rais anapaswa kujua na kujiuliza hili.

Je tunarejeshwa tulikoanzia kwenye kisa cha mchungaji mwizi na mpumbavu? Mwenye ng'ombe alikengeuka na kuustukia upumbavu. Je nasi tutavaa viatu vya mwenye ng'ombe au kugeuzwa majuha mchana kweupe? Mie simo. Kazi kwenu.

Chanzo: Dira ya Tanzania Septemba 2, 2008.

1 comment:

Anonymous said...

Ah! Kusema kweli haya maneno ya hekima!MMMH!!aliyeandika maneno haya lazima nimpe heshima zote!!Nimekubali kazi hii imesimama. I just hope all fisadiz read this!