The Chant of Savant

Thursday 14 August 2008

Ufunuo kwa nchi ya Tanzia

KWANZA namshukuru Mungu kunifunulia yaliyojificha niwaonye wajoli wake.

Tazama, napata usingizi mzito ghafla! Sikutegemea ningelala. Mwenye nyumba anikaba.

Kunidai imekuwa kero. Ana shida. Hivyo shida zake zimalizwe nami! Kama kupata pesa katikati ya wizi wa kitaifa ni mchezo mbona yeye hapati hadi anifuate fuate utadhani kuishi kwenye ubavu wake wa mbwa wa urithi niko peponi.

Hayo tuyaache si peke yangu

Kweli Mungu aweza kila kitu. Amenipa usingizi mnono na maono ili kuwanusuru wajoli wake. Tazama naonyeshwa nchi ya Tanzia ikiwa mikononi mwa fedhuli mmoja maruhuni sharmuta. Ni mtu mwanaume apendaye kujichekeshachekesha lakini hatari.

Fedhuli huyu anaitwa Njaakaya Kikwekwe. Ni mtu mwongo sina mfano. Ni mtu wa kuogopwa kuliko hata ukimwi. Tanzia, kama mzoga wa tembo unaogugunwa na tumbusi, mbwa mwitu, fisi na wadudu unang’aa kwa juu baada ya kupigwa jua. Ndani hamna kitu!

Fedhuli huyu ni Niwewe kweli mwenye kutia kiwewe. Wengine humuita Kiwewe. Jamaa ni machukizo na maanguko. Akisaidiana na mafisi, mbweha na chui, watu wameinajisi nchi ya Tanzia.

Tazama naona hasira za Mungu zikiwashukia wajoli wa Tanzia. Ana maya nao. Wamekubali kuwekwa rumenya na Njaakaya na watu wake. Anawapatiliza kwa kuridhia machukizo. Anawapatiliza kwa kutochukua hatua. Dhambi hii itawatafuna hadi wafanye kweli.

Naona mbwa mwitu wakivaa ngozi za kondoo. Wako mezani mwa fedhuli wakila na kunywa. Wanawahadaa kondoo kuwa watawanusuru il hali wako pale kuwararua.

Naona mbwa fisi wakichunga jokofu la nyama! Mwisho wao ni nini? Wamehongwa mabaki na mapupu kiasi cha kuhatarisha usalama wa wajoli waliwao kama kondoo wapumbavu waliowaamini wawaokoe wasijue lao moja-kuwararua!

Fedhuli ameigeuza nchi ya neema kuwa ya mabalaa. Amewaalika vinyamkera na vinyama vya usiku kuiguguna na kuinajisi nchi. Amepafanya patakatifu pa patakatifu kuwa danguro na nyumba ya uovu.

Nchi ya shibe imegeuka ghafla kuwa kambi ya wajoli wenye njaa ya kila kitu hata mawazo! Nchi ya maziwa na asali imegeuka ya machozi na vilio. Yale maziwa na asali vimegeuka usaha. Nani aliwahi kuonja machozi asikie chumvi yake? Vilio vinasikika kila mahali. Kila mahali ni sura zilizokunjamana. Maisha siyo maisha, si watoto wala wakubwa.

Kinachokera, fedhuli na watu wake waleta majanga wanazidi kuhanikiza wakiwahadaa wajoli kuwa huko waendako mambo yanaweza kubadilika wakati ndiyo yanazidi kuguma!

Wajoli, kwa upogo wa nafsi na akili zao, wanakubali na kuvuta subira. Ni balaa kiasi gani kwa kondoo kuvuta subira akingoja mchinja? Yupi mpumbavu kati ya kondoo achinjwaye akijaribu kuikata kamba lau anusuru shingo yake na yule avumiliaye akijua mwisho wa yote ni nini?

Tazama Mungu mwenye hasira anashusha mapigo kumi kwa nchi ya Tanzia.

Kwanza, gilba na uongo kila namna; wajoli wadanganyika wanazidi kuuamini urongo wakiziba milango ya fahamu wasing’amue uongo na dhihaka wafanyiwao na fedhuli na watu wake.

Pili, uvivu: Uvivu umekuwa ndiyo kila kitu. Watu wazima wenye akili na nguvu wameshindwa kuvitumia. Wamekalia matumaini yasiyokuwapo badala ya kuamka wakapambane na wabaya wao ambao wamo kazini kuwaangamiza. Mungu amewatia uvivu ili baadaye uwahiriki.

Tatu, rushwa: Tanzia ni mama wa rushwa katika bara la kusadika. Kwa juu inaonekana iking’ara. Kwa ndani, hata kaburi lina nafuu. Imetulia sawa na jua wakati ndani ni vimbunga.

Nne, mgawanyiko: Watanzia japo wanajiita ndugu na wamoja, wamegawanyika sawa na changarawe barabarani. Utaziona changarawe ziko pamoja lakini si rahisi kuzishikanisha hadi uzipitishe kwenye moto wa zege.

Tano, umaskini: Mungu kashusha pigo kuu kuliko yote. Nalo si jingine ni umaskini kuanzia ubongoni hadi maungoni. Tanzia inaongoza katika bara la kusadikika kuwa na watu maskini na watawala wakwasi kulihali.

Walijaliwa mali. Lakini wameruhusu wageni kuja kujichotea huku wakiwahonga watawala vibaka na vipofu wa Tanzia bakhshishi. Watanzia ni maskini kuliko hata chawa. Kwani chawa hula kwenye maungo ya wenzake lakini bado akabakia mdudu asiye na ubongo wa kupambanua mambo.

Sita, roho mbaya: Watanzia wameingiwa na shetani wa roho mbaya. Wameanza kuchinjana wao kwa wao kuusaka ukwasi kwa njia za kiza. Katika nchi ya Tanzia matupinkere wako hatarini kutoweka. Badala ya Watanzia kukabili chanzo cha masahibu na msiba wao kuwa ni utawala mbaya wa fedhuli Janga, wamegeuziana wenyewe silaha.

Nchi ya Tanzia inaendeshwa na nguvu za giza kuanzia kwenye nyumba za ibada hadi kwenye vigwena vya wachawi wajiitao waganga. Nchi imemezwa na ushirikina hakuna mfano. Ajabu washirikina na wachawi katika nchi ya Tanzia hufanya uchawi wao hadharani wakiutangaza hata kwenye magazeti na radio.

Kama Misri na Firauni, fedhuli hana wasi wasi. Kwani anajua aina ya wajoli anaowatumikia kujenga mhimili wa machukizo yaitwayo CCM au Chetu Cha Maendeleo ambayo maana yake ni Chenu Chekeni ni Maaanguko.

Saba, wizi: Fedhuli na wezi wenzake wamezishambulia hazina za Tanzia na kuziibia kiasi cha nchi kuendeshwa kama duka la Mwarabu. Nchi iliyosifika kutoa huduma za jamii bure sasa inaziuza. Heri ingeziuza zikiwa ni huduma kweli na siyo utapeli kama ilivyo Tanzia.

Nane, ulevi: Watu wa Tanzia ni walevi duniani hakuna. Heri wangelewa pombe ingepigwa marufuku. Wamelewa matumaini. Wanakalia mkia kama nyau wakidai wamekalia kochi. Nchi nyingi za jirani zimeshindwa kukalika kutokana na machukizo yasiyofikia hata robo ya walevi wa Tanzia wanayofanyiwa.

Tisa ukahaba: Tanzia ni nchi kahaba hakuna mfano. Imewekeza kwenye madanguro na ulevi huku rasilimali za taifa zikisombwa na wageni.

Kumi, utaahira: Watanzia ni mataahira zaidi hata ya hayawani. Wana macho hawaoni. Wana masikio hawasikii. Wapo wapo wasijue wapelekwapo ni machinjioni! Nikiwa nalala. Mara nasikia sauti ikinena ‘busara hii.’

Mzigo wa ujinga siku zote ni mzito. Mzigo wa upumbavu ni mzito zaidi na mzigo wa maarifa wala hauna uzito. Maarifa hurahisha maisha wakati ujinga na upumbavu hufanya hata maisha rahisi kuwa magumu. Mzigo wa upumbavu ni sawa na ule wa zebaki wakati wa maarifa ni sawa na ule wa maji. Mzigo wa zebaki ukipasuka aliyeubeba atauawa na zebaki lakini wa maji utampoza mbebaji.

Mchwa hana mikono wala kichwa cha kubebea ndoo ya maji wala zege. Je, hukoroga na kulisomba zege lake vipi? Ashukuye ukweli huu aangalie kichuguu. Je, kichuguu si nyumba bora kuliko ghorofa? Japo hapewi sifa yake? Ukiondoa miti na milima, mchwa ndiye kiumbe wa kwanza kusimamisha ghorofa kwenye uso wa ardhi. Laiti ardhi ingepata mdomo na ulimi ikasema, ukweli huu ungeuona na cheti cha ithibati ya uvumbuzi wa nyumba za maghorofa angepewa mchwa. Je, kingemsaidia nini wakati hana shida na mali zaidi ya utii wake?

Mchwa hana panga wala shoka lakini huangusha magogo! Je, busara ya mchwa kupewa kiwiliwili kidogo na kichwa kikubwa si ishara ya maarifa?

Heri washikao mambo haya maana yatawafaa. Wayapuuzao yatawapuuza na kutumikishwa na wale wayashikiao. Duniani hakuna jipya bali namna mpya ya kulifanya la kale kuwa jipya. Waulize wanadamu wote. Watakuwa na vitu vipya hata misamiati mipya. Lakini kuna vitu si vipya hata kama vitafanywa vipya. Waswahili hawakuwa na kompyuta wala gari. Walitohoa maneno haya toka kwa walioleta vitu hivi.

Lakini Waswahili hawa hawa hawakuwa na ukame wa utu wala imani za dini. Jina la Mungu linapatikana katika kila kabila na lugha. Sawa na chakula hewa na kifo ni ukweli kwamba Mungu na dini si vitu vipya bali vya kufanywa vipya. Hapa ndipo masilahi ya binadamu yamewekwa juu ya ukweli na uasili wa maumbile.

Chanzo:Tanzania Daima Agosti 13, 2008.

No comments: