The Chant of Savant

Monday 21 July 2008

Kikwete kutotangaza mali ni dalili za ufisadi?

Sasa ni takribani miaka mitatu tangu rais Jakaya Kikwete aingie madarakani kwa mbwembwe chini ya kauli mbinu Kasi mpya, nguvu mpya na ari mpya ambayo imegeuka kuwa kinyume.

Wapo wanaosema ni kasi mpya ari mpya na nguvu mpya kuelekea kwenye ufisadi na kuiangamiza nchi kama hali itaendelea hivi. Hayo si yangu ni yao na Kikwete wao.

Wengi walidhania kuingia kwa Kikwete kungepunguza machungu waliyokuwa wakiyapata baada ya kuhenyeshwa na utawala kidhabu wa rais mstaafu, Benjamin Mkapa na maswahaba zake. Sasa inaonekana wanapata makubwa kuliko ya awali. Kweli ukishangaa ya Mkapa utaona ya Kikwete!

Pamoja na kuonyesha wazi kuwa Kikwete alishindwa kabla hata ya kuanza kazi baada ya kujizungushia watu mafisadi, wengi walimchukulia kama mtu msafi! Lakini hii ilikuwa ni wakati ule kabla ya kuhusishwa na List of Shame ya wapinzani huku taratibu ukweli ukianza kudhihiri kuwa alijua kila kitu kuhusiana na kampuni tapeli ya Richmond iliyomfurusisha rafiki na mshirika wake mkuu waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa.

Na ushahidi unaanza kuibuka kuwa Kikwete alikuwa waziri wa nishati wakati serikali ilipoingia mkataba tata na wa kiwizi wa IPTL ambao umebainika kuwa wizi mtupu. Rejea kukiri bungeni kwa waziri wa nishati William Ngeleja hivi karibuni. Je atawambia nini watanzania kwa hili wakati akiwaaminisha atapambana na rushwa na asifanye hivyo?


Sasa kadri muda unavyokwenda baada ya serikali ya Kikwete kuvurunda na kushindwa kukidhi matarajio ya watanzania, kuna kila dalili kuwa ufisadi sasa unaanza kutawala nchi.


Kwa mfano, ni kwanini Kikwete hataki kutangaza mali zake na za familia yake? Hii maana yake ni nini? Je haiwezi kutafsirika kuwa anafanya yale aliyofanya mtangulizi wake kiasi cha kujikuta kwenye kashfa lukuki zihusianazo na wizi wa pesa ya umma?

Nisingependa kumhukumu Kikwete. Lakini ushahidi wa mazingira unaanza kumuelekea atake asitake. Aliyekula ng’ombe miguu humuelekea.

Kwa mfano, aliahidi asingekuwa na simile na ufisadi. Lakini kadri muda unavyozidi kuyoyoma, anaanza kuonekana Kikwete wa kweli tofauti na yule wa vyombo vya habari na mitandao aliyeonekana kama kipenzi na mkombozi wa watu.

Tutatoa mifano. Amejionyesha kuwa karibu na mafisadi kwa kuwakingia kifua Mkapa na mkewe na marafiki zao huku akimvumilia Lowassa hadi bunge lilipomtimua.

Ameshindwa kurejesha nyumba zetu zilizoibiwa na utawala wa Mkapa. Ameshindwa kuwashughulikia wale waliobainika kutenda ufisadi ambao wameishabainika na kuwajibika kama Edward Lowassa, Ibrahim Msabaha, Nazir Karamagi na Andrew Chenge. Ameshindwa hata kumfukuza kazi mkuu wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa ambaye analalamikiwa sana .

Ameshindwa hata kuwakamata walioko nyuma ya wizi wa mabilioni ya EPA zaidi ya kula njama eti wazirejeshe bila kufikishwa mahakamani!

Ameshindwa kuleta nidhamu ya matumizi ya pesa za umma. Rejea ripoti mkaguzi mkuu wa hesabu za umma ya mwaka 2006 kuwa wizara za serikali zilikuwa vimefuja zaidi ya shilingi bilioni nne bila maelezo.

Ameshindwa kuleta suluhu Zanzibar . Ameshindwa hata kuwa na falsafa ya utawala wake. Ameshindwa na vita dhidi ya mihadarati. Ameshindwa vibaya sana . Ameshindwa kuwakamata wauza unga wanaojulikana! Ameshindwa karibu kwenye kila kitu!

Kuzidi kuona ni kwanini umma unadhani Kikwete ameshindwa kupambana na ufisadi na kufufua uchumu, je ni kwanini Kikwete hakanushi au kukiri madai ya List of Shame iliyoibua kashfa zote tunazoshuhudia leo zikilitikisa na kuliaibisha taifa bila kubakiza utawala wa Kikwete?

Ameruhusu mkewe aunde NGO kama ya Anna Mkapa iliyoishia kuwa kijiko cha kuchotea mali ya umma na kupokelea pesa chafu toka kwa wafanyabiashara wezi. Mara nyingi NGO za wake wa wakubwa hupata pesa nyingi toka kwa wafanyabiashara wachafu wanaokwepa kodi hata kuuza mihadarati. Rejea kwa mfano kwa sasa NGO ya mke wa Mkapa kukosa wachangiaji sawa na Mkapa alipokuwa madarakani. Nani atachangia NGO ya mtu ambaye mme wake hana madaraka tena.

Ameshindwa kukemea migawanyiko ndani ya chama chake kinachohusishwa moja kwa moja na ufisadi na wizi wa pesa ya umma. Rejea kutajwa kwa Deep Green Finance kampuni ya CCM. Rejea kutajwa kwa kampuni ya Meremeta inayohusishwa na wizi wa mabilioni ya shilingi toka Benki kuu.

Kinachoiunganisha zaidi CCM ni madai kuwa pesa husika ilitumika kwenye uchaguzi uliomuweka Kikwete madarakani kupitia sheria chafu iliyoruhusu rushwa maarufu kama Takrima. Hii ni sheria moja chafu duniani kuwahi kutungwa na bunge linalojiita la wananchi dhidi ya maslahi ya wananchi.

Ameshindwa na kukataa hata kuanzisha uchunguzi wa kifo cha gavana wa zamani wa Benki kuu, Daudi Ballali anayedaiwa kuuawa ili kuficha kashfa na siri za wakubwa akiwamo yeye na chama chake. Na kutofanya hivyo kunazidisha ukweli kuwa kweli Ballali alitolewa kafara ili kunusuru wakubwa wachafu.

Ukiachia mbali kuchukua hatua mjarabu, Kikwete ameshindwa hata kukemea maovu yote haya. Amejitahidi kukaa kimya kama njia ya kuusahaulisha umma. Je hili ni jibu? Je watanzania wataendelea kungoja hadi lini ilhali ufisadi unazidi kupanda chati?

Je katika hili nani wa kulaumiwa zaidi ya watanzania wenyewe wanaokaa kimya huku wakilalamika vipembeni? Je serikali inakidhi matarajio ya umma? Kama jibu ni siyo, umma ufanye nini zaidi ya kuiamsha hata kuifurusha? Maana kuwatawala watu ni mkataba sawa na kuajiriwa. Kama mwajiriwa anakutwa hana viwango na ujuzi vilivyotegemea hufukuzwa.

Kinachotia mashaka zaidi ni ile hali ya Kikwete kuendelea kuwapumbaza watanzania kwa kutoa lugha tamu na ahadi nyingine ilhali zile za awali hazijatekelezwa hata moja!

Kwa namna mambo yanavyoendeshwa holela, wachambuzi wanaanza kujiuliza swali moja kuu. Je ni fisadi gani tunayemtafuta? Je tunamwambia awaadhibu mafisadi naye ni safi na ana mshipa wa kufanya hivyo bila naye kuhusishwa kutokana na yake kujulikana?

Kuepuka kumuingiza Kikwete kirahisi kwanza angetangaza mali zake na za familia yake.

Pili angejiepusha kurudia makosa ya mtangulizi wake kwenye utawala wake hasa kuwabana waliomzunguka akihakikisha wote wenye mabaka wanatimuliwa na kushitakiwa.

Kujitenga nao na kuacha kuwakingia kifua wala kusikiliza ushawishi wao. Kuna haja ya kufanya hivyo tena haraka hata kama wahusika kwa michango yao walimuwezesha kuingia madarakani. Je kushindwa kutangaza mali zake na familia yake, Kikwete hajengi mazingira ya kuonekana fisadi?

Source: Dira ya Tanzania Julai, 2008.

No comments: