The Chant of Savant

Wednesday 11 June 2008

Wanalinda maiti inayonuka!

TANGU niache gongo na bangi sikosi ufunuo. Japo si mtume kwa taifa maalum, huwezi kujua. Imeandikwa; walitumwa mitume kwa maelfu. Utajuaje ni mmojawapo? Isitoshe, kila mkataza mabaya akaamrisha mema, ni mtume hata kama haingii msikitini au kanisani.

Si haba, Mpayukaji ni mtume kwa taifa lililodanganyika na kupotea, na ana kila dalili na ushahidi kuthibitisha utume wake. Tuyaache tusije kupigana mawe bure na kutishiana mashingo.

Katika ufunuo niko kwenye nchi iitwayo Tanzia katika mji wa Kufa-as salama. Na huu ndiyo ufunuo. Tazama naona maiti anayenuka akiwa amezungukwa na walinzi waliokonda wakimlinda asikamatwe na kundi la wajoli wenye hasira anaotaka azikwe kuondokana na harufu mbaya na wadudu vimtokavyo maiti huyu.

Pembeni naona mifupa mingi ya watu iliyokauka, inasemekana ilikuwa imeliwa na huyu maiti na wenzake waliokuwa wamewatupia wale askari mithili ya mbwa wamlindao wagugune kama takrima yao.

Wajoli wamehanikiza wakisema: "Azikwe, azikwe tena leo." Mara mkuu wa wale walinzi waliokondoena kwa njaa na dhiki na magonjwa naye anasema: "Nani hapa, nyie si maiti watarajiwa kama mimi?"

Anaendelea: "Muoneeni huruma mwenzenu apumzike kwenye ufu wake. Na liwalo na liwe hazikwi maiti hapa."

Japo kuna wanaomshangaa kwa nini mtu mzima anafanya istizimari hadi kulinda uoza na harufu mbaya wasijue naye alishaugua na kuanza kunuka taratibu! Naye ananuka ingawa amejitona uturi. Anatema wadudu wakavu.

Naona wajoli waliochukia wakimgeukia mkuu na kusema: "Nawe unanuka na tunajua u mfu mtarajiwa kitambo si kirefu. Wewe na nyumba yako mmeishapigwa na majipu ikiwa ni alama ya laana ya kurithi na kuendeleza usaliti wa taifa la Mungu."

Maskini maiti na mkuu wa walinzi. Hawakujaliwa kuota ndoto na kupokea ufunuo! Hawajui, ingawa, wanalindwa bado ni maiti wa kesho! Hajui kuwa wanajua anaugua ugonjwa wa majipu anayoficha kwenye mavazi yake ya thamani! Hajui umma unajua hayo ndiyo matokeo ya laana ya kuhujumu umma!

Japo mkuu ana macho, ukweli ni kwamba ni kipofu asiyeona zaidi ya usawa wa tumbo na pua yake. Maana ni jana tu huyu maiti mtoa harufu anayemlinda alikuwa hai, lakini akalaaniwa kutokana na kula nyama za wenzie huku akijitia kiburi na ushufaa asijue zake zilikuwa zimeisha!

Maskini hajui maiti wake wanayetaka azikwe alikufa kwa ugonjwa huu! Ugonjwa huu uliuua ukoo wake. Ulimuanza yeye. Ukafuatia mkewe, wanae, mashemeji zake hata marafiki. Baya zaidi, alimuambukiza rafiki yake baada ya kumuachia makapi yake ayale!

Hawakujua. Mkuu huyu hata baadhi ya walinzi aliwarithi toka kwa maiti wanayetaka azikwe ilhali mkuu akimlinda kwa gharama yoyote akijua naye kesho yatamkuta!

Wakati nikiendelea kutafakari vita baina ya waja, wagonjwa na marehemu, mara niliona kundi la mbwa na inzi likishabikia harufu ya ile maiti. Pia yalishangilia uamuzi wa mkuu wa walinzi wa maiti kuiacha bila kuizika ili yaendelee kufaidi uoza!

Ni mbwa na mainzi manono ya rangi ya kijani. Yametapakaa kila sehemu kiasi cha kuvuma na kutoa mlio ulioshinda nguvu ile sauti ya wajoli waliotaka maiti izikwe.

Ghafla ajabu ilitokea. Ile maiti, kwa nyodo, ilianza kupayuka ikikana kuwa ilikuwa maiti! Ilisema wanaosema ni maiti apaswaye kuzikwa ili kuondoa harufu ni wale ambao eti walinyimwa kitowoe cha nyama ya watu wakati wa uhai wake, waliokwenda kwake kutafuta vinono akawanyima! Maiti ilitoa wadudu kila ilipopayuka. Ilipayuka kama imepagawa isijue ni maiti.

Nilishangaa kuona maiti ikiongea tena kwa jeuri. Baadaye niling’amua kuwa ilikuwa ikipata kiburi kutokana na kulindwa na walinzi wa yule maiti mtarajiwa. Ilipata kiburi kutokana na kushangiliwa na mainzi ya kijani.

Kutokana na kiburi cha kuzungukwa na mbwa na walinzi watiifu kwa maiti mwenzie mtarajiwa, maiti ile ilihanikiza ikikana kuwa haikuwa inanuka bali wale waliokuwa wakisema ndio wanaonuka! Iliwakejeli waliotaka izikwe ili kuondoa harufu iliyokuwa ikiwakera. Ilipayuka: "Waongo, waongo, waongo mie sinuki wala si maiti."

Maiti ikiwa inashangiliwa na mainzi ilipaaza sauti na kusema: "Nyie mlikuja kwangu wakati wa uhai wangu mkitaka niwaneemeshe msiwe maiti kama mimi nikakataa sasa mnanionea wivu."

Ilizidi kutema wadudu na harufu kiasi cha kuzidi kuwachukiza wale wajoli waliozidi kuhanikiza izikwe ili kuondoa makufuru na harufu katika ardhi takatifu inayonajisiwa na maiti hawa wawili mfu na mtarajiwa.

Ajabu maiti ile ilikuwa imefura kwa kuchimbwa chimbwa na wadudu! Ilizidisha kiburi baada ya kuona mkuu wa walinzi na mbwa wakiilinda. Mara naona nyuki nao wakiungana na wajoli kutaka maiti izikwe.

Mainzi yalishangilia kusikia maiti ikijitetea. Yalishangilia yakijua kuwa kama ingezikwa yangekosa uhondo wa harufu yake ambayo ni machukizo kwa walio hai, lakini burudani kwao.

Maiti mtoa harufu ilisifika kwa uchoyo na roho mbaya ilipokuwa hai. Ndiyo maana baada ya kufa ilipewa adhabu ya kuwa kituko kwa walio hai. Alisifika kwa usahaulifu wake. Maana kama si yule babu aliyemlea wala asingefikia kuwa mkuu wa umma aliyeguguna na kuacha nyuma dhiki na makufuru. Ajabu aliguguna mifugo hata watu!

Lakini yote aliyasahau akafuata njia ya waovu akiongozwa na maiti wengine na mkewe marehemu ambazo nazo hazijazikwa kutokana na kuzungukwa na wale mbwa wa mfuga mbwa marehemu mtarajiwa.

Tazama nikiwa nashangaa jeuri ya maiti na kelele za inzi na mbwa, mara niliona genge la mbwa mwitu wenye sura za watu likiwa linaguguna kila kitu. Ni mbwa waliokuwa wamenona na kunawiri sina mfano. Ni mijibwa kweli kweli.

Nikiwa natafakari hili na lile, mara niliwaona wale mbwa wanaomlinda maiti anayeshabikiwa na mainzi huku akizomewa na wajoli, nao wakianza kung’aka kwa hasira baada ya kugundua kuwa kumbe kwenye mchezo huu wa mauti waliokuwa wakifaidi si wengine bali mfuga mbwa na mainzi, lakini si wale mbwa.

Mbwa wanaanza kujitambua kiasi cha kuacha kuwabwekea hata kutishia kuwararua wale wajoli wanaodai maiti ile izikwe mara moja.

Tazama naona maiti imezidi kufura kwa hasira ikisema inasingiziwa kunuka na kufa ilhali inayonuka ni maiti iishiyo kwa hisani ya mfuga mbwa mpumbavu anayewatumia mbwa kuwahini na kuwashambulia wajoli badala ya kuwalinda!

Nikiwa nakaa vizuri kutafakari, mara harufu ya ile maiti inaniingia puani. Mara na wadudu waliokuwa wakimtoka wananinyemelea. Ghafla naota nikitimka mbio kwenda kutafuta kolego nizike maiti. Salamu kwa Mzee Machungi Mgosi wa Mtibwa na wanakijiwe wote. Namtaka Mgosi twende zetu Ushoto tukatafute tunguli tuwafunge macho walinzi na mbwa na mkuu wao ili maiti yetu izikwe. Yameadhirika vya kutosha.

Nawashaurini watoke kwenye kibuhuti waje tuzike maiti iache kutunukia. Hakika huu ni ufunuo kwa wenye akili na taamuli. Kwa wapumbavu ufunuo huu ni machukizo. Maana inzi mpenda uoza ukipiga uturi lazima akuchukie. Je, maiti yetu itazikwa au?

Kila la heri.

Source: Tanzania Daima Juni 11, 2008.

1 comment:

Anonymous said...

Kweli wewe ni nabii na huu ni unabii.