The Chant of Savant

Wednesday 18 June 2008

NEC imeamua kuwa chaka la mafisadi?

TAARIFA kwamba Waziri Mkuu mfukuzwa, Edward Lowassa, hakuwa na hatia bali alijiuzulu kuwajibika, ila hakuhusika katika kashfa ya Richmond, ni upuuzi wa mwaka.

Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (NEC) iliyokutana hivi karibuni ilitoa tamko hili la kuchusha na kukera kama lilivyokaririwa na vyombo vya habari.

Inashangaza na kukatisha tamaa kama chama kinachojidai kupigania masilahi ya Mtanzania kikiimba wimbo wa maisha bora kinaweza kuja na upuuzi kama huu! .

Kama hakuhusika na kashfa ya Richmond ni kwanini alijiuzulu? Je, ina maana taarifa nzuri ya kamati teule ya Bunge iliyoongozwa na Dk. Harrison Mwakyembe ni upuuzi?

Je, kitendo cha NEC si kulidharau na kulitukana Bunge na kulionyesha kama taasisi inayosema uongo? Je, Bunge limechukuliaje shambulio na kashfa hii? Kama Lowassa hakuhusika na Richmond, alijiuzulu kwa kosa gani au kashfa gani? Huu ni uchovu wa kisiasa usio na mfano. Huu ni mwanzo wa kifo cha CCM!

Badala ya Kamati Kuu ya CCM kufanya kazi za umma ilifanya kazi ya kusafishana. Na hii si mara ya kwanza kwa CCM kufanya hivyo. Mwanzoni akina Lowassa na wenzake walitaka kuitumia Tume ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) .

Nayo bila tahadhari wala kuona mbali ilijaribu kuwasafisha mafisadi hawa bila mafanikio hadi Bunge lilipoamua kuunda kamati iliyoweka historia ya kuwa Bunge la kwanza katika Afrika kumtimua mkuu wa shughuli za serikali bungeni, waziri mkuu.

CCM imekuwa ikipewa kila aina ya majina mabaya kutokana na maamuzi yake mabaya yaliyojikita kwenye kulindana na kubabaisha. Hivi ni Mtanzania gani awe hata mwanachama wa CCM damu asiyejua kuwa Lowassa alifukuzwa kazi na hakujiuzulu? Ni nani hajui kuwa kilichomfukuzisha Lowassa ni ufisadi wa nyuma ya Richmond? .

Kuna siku CCM watakuja kutwambia kuwa Tanzania ni nchi iliyoendelea. Maana wanaweza kujipayukia lolote kana kwamba wanawaambia ‘mataahira’! Baya zaidi wanapodanganya wanajidanganya na wao pia!

Kama tamko la NEC halitatenguliwa, basi hakuna siri, aliyosema Mwalimu Nyerere yanatimia. Mwalimu aliwahi kuionya CCM juu ya kuvamiwa na wafanyabiashara. Wakati ule tulijua wafanyabiashara, tusijue ni mafisadi.

Je, Mwenyekiti wa chama, Rais Jakaya Kikwete anapotuambia ana azima ya kupambana na ufisadi ilhali akikalia kiti kwenye kamati inayopitisha upuuzi na baraka kwa mafisadi, tumweleweje? .

Tunaambiwa kuwa hata waziri Nazir Karamagi na Ibrahim Msabaha, hawakuwa na kosa! Mbona Msabaha aliiambia Kamati Teule ya Bunge kuwa Richmond ulikuwa mradi wa waziri mkuu wa wakati ule na Mwarabu wake? Kwa nini NEC wamesahau kuwa yaliyoandikwa huwa hayaozi (scripta manenta)?

Kama CCM itashikilia upuuzi huu ningeishauri tume teule ya Bunge na Bunge lenyewe kwenda mahakamani kupinga dharau hii na matusi kwake.

Kama Lowassa na wenzake hawakuwa na hatia wala kushiriki kwenye uchafu wa Richmond, basi NEC ituambie nani wako nyuma ya Richmond. Au ni yale yale kuwa Richmond inafutikwa chini ya busati kuepuka kumtaja mhusika wa kweli aliyeiidhinisha? Je, Watanzania nao kwa upande wao watakubali kugeuzwa mabwege kiasi hiki ilhali kila kitu kiliwekwa wazi mbele yao na kamati teule ya Bunge? Enyi Watanzania ‘wapumbavu’, nani aliwaroga hadi mkaaminishwa kuwa Lowassa na wenzake hawakuwa na hatia bali waliwajibika? Mbona Lowassa na wenzake waliwekwa ‘uchi’ mbele zenu mkajionea na kusikia kila kitu! Namna hii inatisha na si vibaya kusema: Sasa, rasmi CCM imeikabidhi nchi kwa mafisadi .

Tuliwahi kuonya kuwa CCM, kwa sasa ina ombwe la uongozi wenye akili timamu. Tulionya kuwa uchafu wa wakuu wa CCM utaiangamiza nchi. Kweli kama Lowassa hahusiki na Richmond, ni kwa nini ametupwa nje? Je, hii inaweza kuwa janja ya kumsafisha ili arudishwe kwa mlango wa nyuma? Je, uswahiba wake na Kikwete umeshinda hata haki? Je, akirudishwa, Watanzania watamkubali na kumpokea? Maana, kupitia wapambe na ‘waganga’ wake aliwahi kukaririwa bila hata chembe ya aibu akijilinganisha na mzee Ali Hassan Mwinyi aliporejea kwenye siasa na kuwa rais baada ya Wizara yake ya Mambo ya Ndani wakati ule kukumbwa na kashfa ya mauaji ya kina Nzegenuka .

Hivi karibuni Katibu Mwenezi wa CCM, John Chiligati, alikaririwa akipindisha maneno ya tume teule ya Bunge kuwa waziri mkuu wa zamani Lowassa, apime na kuamua la kufanya. Baada ya Lowassa kupima aliamua kujiuzulu. Je, huyu kama aliamua mwenyewe kujiuzulu kama tunavyoaminishwa, hii si ishara ya kukiri kuwa alifanya makosa? Kinachonichefua zaidi ni ile hatua ya NEC kuwamwagia sifa mafisadi shutumiwa waliojiuzulu kuwa walikiletea heshima chama hicho! Je, maana yake hii ni nini? Au ni yale kuwa Lowassa aliamua kuachia ngazi ili serikali yote isianguke? Kama Lowassa aliubeba msalaba wa serikali chafu inayonuka, basi iwe ni kwa faida ya walioko nyuma ya kashfa hizi na si kuwahadaa Watanzania kuwa Lowassa na wenzake hawakuwa na makosa .

Kama CCM ingekuwa ni ile ya Nyerere, Lowassa na wenzake walipaswa kufukuzwa kwenye chama hapo hapo na kuchukuliwa hatua za kisheria, badala ya kumwangiwa sifa za uongo na NEC. Kama kuna kitu kimefanywa na NEC kwa kuwatetea na kuwapongeza kina Lowassa, si kingine bali kuonyesha sura halisi ya Kikwete, wenzake na CCM.

Kinachoonekana hapa ni kwamba CCM sasa ni chama cha mafisadi. Kinachojibainisha hapa ni kwamba pesa iliyoibwa na hawa watu na washirika wao si chochote, isipokuwa ushindi kwa CCM! Je, CCM imewapongeza hawa mashujaa wake kutokana na kazi yao njema ya kulihujumu taifa ili CCM ishinde kupitia takrima? .

Kama si hivyo, sasa ni nini kilichoishawishi kamati kuu kufanya upuuzi wa mwaka? Je, wajumbe nao walihongwa kiasi cha kuja na usanii huu usioingia akilini?

CCM sasa inafikia ukingoni. Katika kikao hiki cha NEC, tunaarifiwa kuwa kulikuwa na mgawanyiko. Wana CCM safi walitaka mafisadi wasulubiwe huku wakubwa wao wakiwapinga. Je, wadogo walilazimishwa na wakubwa kuridhia upuuzi huu? Je, NEC imeamua kutoa taarifa yake na si ya wajumbe? Maana hatujaambiwa jinsi walivyofikia kutoa tamko hili hatari kwa nchi na hata kwa chama chenyewe

Je, wale wana CCM safi watakubali kuburuzwa na kuonekana wasaliti kwa taifa lao kwa kuogopa wakubwa wao? Je, tutegemee nini? Wapo watakaojitenga na CCM kuhakikisha haki inatendeka au nao watageuka wanafiki na wachumia tumbo kiasi cha kukubaliana na jinai hii? Hata kama CCM itazika tofauti zake kwa ujanja au nguvu, ukweli ni kwamba ina nyufa nyingi kiasi cha kushindikana kuzibwa. Na hili likiongezewa na kuwa na uongozi mgando usio na visheni wala udhu, siku za CCM zinaanza kuhesabika .

Kama imeweza kutekwa na kushindwa na kundi la wahalifu wachache, kweli kitaweza kupambana na changamoto za kuendesha taifa kubwa kwenye karne hii ya sayansi na teknolojia, ambapo kashfa za wateule wake zinavujishwa kwenye mitandao kila uchao? Je, huu ni mwanzo wa mwisho wa CCM? Nani anajua? Tuhitimishe: Taarifa ya Kamati Kuu ya CCM ni matusi na kejeli kwa Watanzania. Inapingana na anayotuaminisha kila uchao Rais Jayaka Kikwete na mwenyekiti wa CCM. Hakika chama hicho kimegeuka chaka la ufisadi .

Je, kwa CCM hii ya mafisadi tutaweza kuushinda ufisadi na kuwaletea Watanzania maisha bora? Kama CCM inataka kurejea kwenye uchaguzi ujao, basi badala ya kuwasafisha mafisadi, ije na hoja ya kuwabana warejeshe pesa yetu na kushitakiwa kwa ufisadi.

Isiharibu ushahidi utokanao na kuwajibika kwao. Na kama kuna ndoto ya kumrudisha kwenye ulingo wa siasa yeyote kati ya wale tuliokwisha kuwatimua, ijulikane ni ndoto ya mchana.



Source: Tanzania Daima Juni 18, 2008.

2 comments:

Anonymous said...

good job

Anonymous said...

Blogger crackdown
More bloggers than ever face arrest for exposing human rights abuses or criticising governments.


A report from the University of Washington says 64 people have been arrested for publishing their views on a blog in the past five years.


More than half of them are in China, Egypt and Iran and many serving jail time.


Blogger arrests hit record high

LINK:
http://www.bbcworld.com/Pages/ProgrammeFeature.aspx?id=18&FeatureID=27