The Chant of Savant

Wednesday 13 February 2008

Niliota nachonga na Nyerere.

TULIMWITA Mchonga kutokana na kuchonga meno. Naye alikubali meno na maneno yake yalikuwa yamechongwa kweli. Yote katika yote, maneno yake yemeendelea kuchongoka na kuwachoma mafisadi, tena kwa namna na wakati ambavyo havikutegemewa!

Kwanza leo niko peke yangu kijiweni, nilivyo na usongo we acha tu. Nikiwa nimetoka kuutwika kwenye sherehe za kujipongeza kutokana na ukweli kudhihiri na baadhi ya mambo kuwekwa hadharani, niliamua kuupiga usingizi baada kupiga vifijo na kushangilia si kwa sababu ya kumchukia yeyote bali matendo yao.

Nikiwa ndiyo nimeutwika kutokana na ofa za wenye nazo siku hiyo, niliingia kitandani kwa furaha. Maana hata mshirika wa 'bedroom' si haba. Siku hii alionekana kufurahi akiwa na matumaini mapya kuwa huenda nchi yake itarejeshwa mahala pake.

Kwanza niwaonye. Msizowee kuota kama mimi au wengine walioota kuwa wao watakuwa wao katika kila kitu, hasa lijapo suala la ulaji wa njuluku za wadanganyika waliokufa wakimlilia Mchonga.

Ndoto ilikuwa hivi. Niliota nasalimiana na Mwalimu Julius Nyerere akiwa mwenye furaha. Eti alinishika mkono kwa furaha akinipongeza kwa kurithi kipaji chake cha kuchonga. Alisema. "Kijana, hata kama huna jukwaa la kisiasa, una jukwaa la kalamu. Kweli kalamu yako na wenzako ni kali".

Alitabasamu nikaona yote thelathini na mbili yakiwa meupe pe kama kawaida yake. Alisema. "Mwanangu kwa miaka yapata kumi nilikuwa na simanzi sina mfano. Hata akina Edward Sokoine, Seth Benjamin na Mkwawa walikuwa wakisononeka. Lakini leo nina furaha na nakutaarifu: lipo jambo nililosema miaka 14 iliyopita.

"Lakini bahati mbaya hamkunielewa. Siwalaumuni. Ni uteke na uchanga wa mambo kwenu hasa nyinyi vijana wa sasa msiosoma historia na mambo mengine yanayoendana na dunia yenu yenye kila ya changamoto." Alinikazia macho na kucheka kwekwe kwe. Nami sikujivunga. Niliungana naye nikacheka kwa sauti. 'Kwa kwa kwa.' Mwalimu anaendelea. "Nilisema nikapuuziwa. Wengine waliniona kama mzee mjamaa. 'What a mistake'! Walisahau kuwa utu hauna ujamaa wala ubepari. Nasema tena bila kufumba. Yuda atatiwa msalabani mbele ya Lucifer. Nilisema na nitasema.

Mama Maria na Rashidi mashahidi. Kila jiwe linapaswa kufunguliwa. Maana bado uchafu upo na ni mwingi ukiachia mbali hii kulindana." Ananuna na kuzidi kunikazi macho hadi napata taabu nilipokuwa.

Anaendelea. "Niliweka mfumo safi chini ya azimio. Chini ya Azimio la Arusha. Niliweka mfumo safi sana kabisa. Walikuja wahuni wakauvuruga na sijui Azimio sijui Angamio la Zanzibar. Hawa ni wahaini. Walipaswa kukamatwa na kufungwa. Walivuruga nchi hawa." Anakohoa huku akiwa anazidi kukunja uso na kuendelea.

"Leo watu wangu wamekata tamaa hadi kusema nchi imeoza. No. No. Nchi haijaoza. Waliooza ni wao. Unawaona walivyooza kijana? Pale. Pale Ikulu nilionya. nilionya pale Ikulu pamegeuka pango la wezi. Nilionya pale ni patakatifu. Kuna nini sasa? Naona wahindi, waarabu na wengine.

Kumekuwa kama pale Magomeni kwenye karata tatu! Wasiowatakatifu wakienda patakatifu wakafanya yasiyo matakatifu watapachafua patakatifu. What is this? Kijana nakuuliza. What is this? Hii inachukiza sana.

"Watu wachafu kuingia patakatifu inachukiza. Zamani wakati wa Musa, mtu mchafu akiingia patakatitu akapanajisi adhabu ilikuwa ni kwa taifa zima. Wakati ule tukisoma pale Tabora, mwalimu wangu Mzungu Mr. Denis alizoea kusema: God was less mercy for the messy." Anacheka tena na kuendelea. "How come watu wazima wafanye mambo ya kitoto halafu waje kutudanganya na kutufanya wapumbavu? Anayekudanganya hukufanya wewe juha kama yeye." Anatikisa kichwa na kuendelea.

"Pale Mwitongo ni mbwa. Ni mnyama wa ajabu sana! Jamaa yule hulinda mali zangu kila siku. Ajabu hadai mshahara zaidi ya mifupa, mapupu, makanyagio na makombo. Huyu ni hayawani hawezi kusema, kudai wala kulalamika hata kama anaumia. Huyu ni mbwa. Watu ni watu. Huwezi kutendea watu kama mbwa ukawa nawe mtu. Watu hutendewa kiutu. Anayewatendea watu kama mbwa naye hanusuriki. Watu ni watu hata kama mliwadanganya kwa takrima."

Anafikicha mikono na kuendelea. "Where and how did you get this money? Mlinunuliwa nao mkawanunua. Mlinunuana na kuchuuzana. Mlichuuza roho na miili yao hata yenu. Leo mnakaangana na kuchuuzana zaidi. You’re vending each other.

Leo mtakamata huyu. Kesho mtakamata yule. Lakini bado tatizo litaendelea kuwapo kama hamtatumbua donda zima. Huwezi kuchezea haki na utu ukanusurika. Kama utanusurika ni kwa kitambo kidogo tu nasema. Haki mnaweza kuchezea kuuza hata kununua. Lakini mwishowe-mwishowe mtaumbuana na hata kutoana kafara. Juzi nilisikia maneno ya ajabu kabisa. Sikuwahi kusikia 'bangusilo'. Hata kidogo. Na bado. Kwe kwe kwe!" Anacheka.

"Wazanaki wana ngoma. Kwa Kiswahili nii niii, sema au pasua. Ndiyo. Pasua. Katika ngoma hii watu husutana hasa watemi pale wanapotenda mambo ya hovyo. Mtemi husutwa hata kusemwa mambo yake ya ndani kama atafanya mambo ya hovyo.

"Baba yangu alikuwa chifu. Alikuwa chifu. Mtu safi kabisa anayeheshimiwa na wote. Anayejiheshimu na kuheshimika. Hakuwahi kuimbwa wala kuimbiwa nyimbo za hovyo za pasua. Si yeye wala naibu wake.

Leo ukiona naibu wako anaimbiwa pasua jua umeimbiwa wewe. Maana yeye anakuwakilisha wewe. Ukiona kavuliwa nguo jua umevuliwa wewe.

"Jivue uchafu kuliko kuvuliwa nguo. Haya yanatokea na yatatokea sana kama watu wataendelea kufanya mambo ya hoovyo. Ndiyo. Ndiyo. Wapo vijana mahiri. Wamesoma na kuelimika. Wanajua kuandika. Wanajua kujenga hoja na kuzitetea. Hawaabudii pesa wala rushwa hawa.

"Ni vijana safi wa azimio hawa. Ukiowana au kuwasikia utawajua. Waliua azimio wasijue wanajiua. Hawa ni vipofu. Ni vipofu hawa. Maana hawakuona mbali zaidi ya kuishi kutumbukia kwenye kaburi walilojichimbia wakidhani wanawachimbia Watanzania."

Anatoa leso yake mfukoni na kujifuta mdomo na kuendelea. "Hawa walaaniwe na kusakwa popote walipo na kuonyeshwa cha mtema kuni. Ndiyo ndiyo. Watafutwe na kudhalilishwa, kufilisiwa ili wengine wasirudie jinai hii.

"Hii nchi ni ya wananchi. Siyo ya vibaka na malaya wa kiuchumi na kisiasa. Ndiyo. Maana malaya hujiuza kwa yeyote bila kujali ukubwa wala udogo wake."

Nikiwa naendelea kufaidi mawaidha adhimu na adimu ya Mwalimu mara mshirika wangu wa 'bedroom' alinitingisha ili aniulize jambo fulani mara nikakatisha ndoto yangu. Nilikuwa nikitokwa jasho hadi pombe iliniisha.

mpayukaji@yahoo.com

Source: Tanzania Daima Februari 13, 2008


No comments: