The Chant of Savant

Monday 18 February 2008

Biashara na siasa: Kikwete anajichanganya

NIANZE makala hii kwa kueleza msimamo wa serikali kuwa tangu kuingia kwa sera babaishi za kukopa za ubinafsishaji na za ugenishaji, serikali ilitamka wazi bila kulazimishwa kuwa inajitoa kwenye biashara.

Serikali ilifanya hivyo ili kushughulikia usimamizi wa dola, ingawa hata katika hilo nako inaonekana imechemsha na kuzidiwa kete, kutokana na kuwa na watendaji wafanyabiashara.Kitu ambacho sielewi ni kama serikali ilijitoa kwenye biashara ili watendaji wake wajiingize kwenye biashara?

Taarifa za vyombo vya habari za Februari 6, mwaka huu kuwa Rais Jakaya Kikwete ataandamana na wafanyabiashara 67 ziarani Ujerumani, zimenichanganya licha ya kunitatiza. Hayo yalisemwa na Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Emmanuel ole Naiko, wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Siku chache kabla ya ujio wa habari hii, Rais Kikwete alikaririwa na vyombo vya habari akiwaonya mawaziri na wabunge wachague kati ya siasa na biashara.Alisema kufanya biashara na siasa au siasa za biashara au biashara ya siasa huleta mgongano wa kimaslahi, kiasi kwamba kuzua wasiwasi kwa wananchi wanaotegemea watendaji hao hao wawatumikie badala ya kuwatumia kutengenezea pesa na utajiri binafsi.

Kabla ya kusema hayo, mapema mwaka jana Rais aliandamana na kundi la wafanyabiashara kwenye ziara yake nchini Marekani.

Kama sikosei, alichosema Rais kuhusiana na biashara na siasa kinakinzana na alichokifanya mwaka jana na anachotarajiwa kukifanya mara tu baada ya kuonya siasa za biashara.

Hii si mara yangu ya kwanza kumuonya Rais kujiepusha na wafanyabiashara. Kumuonya kwangu kutokana na yanayomkuta sasa mtangulizi wake, Benjamin Mkapa, ambaye anatuhumiwa kujipatia utajiri akiwa Ikulu kiasi cha kukiuka maadili ya uongozi.

Watu wengi wamekuwa wakimuita 'rais msanii' kutokana na kusema hili leo na kesho akafanya kinyume na hilo alilosema.Wanamuona hivyo kutokana na staili yake ya kuongoza ambayo unaweza kuiita ‘laissez-faire’ kwa lugha ya kigeni. Maana yake ni kusema au kufanya lolote bila kujali kama anajipinga au anakosea.Rejea kauli yake kuwa anapata taarifa nyingi za ufisadi kwa simu yake ya kiganjani. Alipobanwa ilionekana kuwa alikuwa akiongopa, kwani hata waandishi wenyewe aliokuwa akiwaambia hawakuwa wanajua namba hiyo. Hadi leo hajawahi kuweka wazi 'namba' yake hiyo!

Tukio jingine kama hili ni pale alipodai anayo majina ya wauza mihadarati. Hadi naandika hata baada ya kufa kwa mbunge kijana aliyejulikana kwa upambanaji wake dhidi ya mihadarati, Amina Chifupa, Rais - kwa sababu anazojua mwenyewe - hajawahi kukamata lau mmoja wa vigogo hao wa mihadarati!Tulidhani, baada ya Rais kumpoteza mbunge kijana kama yule angetoka usingizini na kufanya kweli, lakini wapi!

Tukirejea kwenye uswahiba na ukaribu wa Rais na wafanyabiashara, tunapata shaka na ‘seriousness’ ya Rais. Kwa nini wafanyabiashara? Je, hii inathibitisha madai yanayotolewa mara kwa mara kuwa alichangiwa na wafanyabiashara kuingia madarakani?Ni vema akumbuke kwamba ushindi wake wa tsunami inayotutokea puani, uliwezeshwa na wakulima na wafanyakazi wa nchi hii na si wafanyabiashara hata kama walichangia chama chake.

Rais inabidi afahamishwe kuwa wafanyabiashara wanapaswa kushughulikia dili zao bila kubebwa na Ikulu. Kwa nini Rais anapendelea kubeba mzigo usio wake na wenye kumtia kwenye vishawishi, kiasi cha kukosa imani na wananchi wanaoona jinsi wafanyabiashara walivyo karibu kila kwenye kashfa inayowahusisha watawala wetu? Rejea ushoga wa rais wa zamani Benjamin Mkapa na gavana wa zamani wa BoT, Dk. Daudi Ballali na akina Jeetu Patel.

Rejea ushoga baina ya waziri aliyesaini mkataba tata na kampuni Richmond inayotuhumiwa kutuibia pesa yetu na wenye kampuni hiyo.

Kwa nini iwe vibaya kwa mawaziri na wabunge kuachana na biashara na kufanya siasa au kufanya biashara na kuachana na siasa, lakini hapo hapo iwe vizuri kwa rais kujizungushia wafanyabiashara kwenye ziara zake?

Kuna haja ya kuinusuru nchi na rais wetu kutoka kwenye mikoba ya wafanyabiashara. Kuna haja ya kumuondoa rais wetu kwenye uchuuzi na kumrejesha kwenye urais. Kama anavyoona mgongano wa kimaslahi kwa mawaziri na wabunge kufanya siasa na biashara, nasi tunaona mgongano huo huo kwenye ushoga na wafanyabiashara.

Anachofanya Rais kinathibitisha ukweli kuwa CCM, chama tawala kinachounda serikali tawala, kimenasa kwenye mikoba ya wafanyabiashara.Rais, ambaye ni mwenyekiti wa chama hicho, angekuwa wa kwanza kuona madhara na lawama kinachopata chama chake kutokana na kukumbatia wafanyabiashara ambao hatima yake wamekitumbukiza kwenye kashfa kama ile ya BoT.

Wafanyabiashara wanafanya biashara kujineemesha binafsi na familia zao. Rais amechaguliwa kuneemesha wananchi wote kwa usawa, kuanzia wafanyakazi, wakulima na wengine. Na isitoshe nchi yetu ni ya wakulima na wafanyabiashara na siyo ya wanasiasa na wafanyabiashara.

Kama kuna uhitaji maalumu wa serikali kushughulikia biashara na wafanyabiashara basi ushughulikiwe na waziri wa biashara na si Rais wetu.

Itakuwa jambo la kipuuzi, kuona Rais anaandamana na wacheza mpira au muziki ilhali kuna wizara ya mambo haya.

Mwalimu Nyerere alituachia mwongozo wa urais hata kama siyo rasmi. Yeye, kama Yesu, alijitenga na kuigeuza Ikulu kuwa pango la wezi, yaani watoza ushuru na wabadilisha pesa ambao katika mada hii ni wafanyabiashara.

Kwa nini tunakuwa wagumu wa kujifunza? Kwa nini hatutaki kuliona lililotaka kumgharimu mamlaka yake, makamu wa rais wa zamani wa Afrika Kusini, Jacob Zuma?

Kwa nini Rais wetu ageuzwe ‘advertisement manager’ wa wafanyabiashara? Kwa nini bendera yetu itumikie biashara badala ya umma?

Kama rais hajui basi ajulishwe. Tujalie kwenye wale anaoandamana nao, wamo wanaotuhumiwa katika kashfa mbalimbali za ufisadi zilizogubika taifa letu.Haoni itakuwa vigumu wahusika kuchunguzwa? Watachunguzwa vipi iwapo ni washikaji na washirika wa rais? Tunajifanya kama hatuijui nchi yetu.Kwa nini rais anashindwa kujifunza kutoka kwa rais wa awamu ya pili, Mzee Ali Hassan Mwinyi ambaye wafanyabiashara walitaka kumtia matatani kwa kisingizio cha kununua kila kitu chake hata leso ya kamasi?

Nani amesahau wafanyabiashara wenye madoa walipofikia hata kumwita shemeji mke wa rais (First Lady), kiasi cha kuwatia kinyaa na kichefuchefu Watanzania wenye rais wao?

Kama rais ameridhika na chama chake kubinafsishwa kwa wafanyabiashara kutokana na sera zake chovu, basi asibinafsishe nchi yetu kwa wafanyabiashara ambao wameishatutia msambweni.Ni upuuzi kwa mtu kung’atwa na nyoka kwenye shimo lile lile mara mbili.

Katika hili, haiwezi kujengeka dhana kuwa rais anawatumia wafanyabiashara anaoandamana nao kuficha biashara zake?

Tuzinduke usingizini tuzuie rais wetu kutekwa na pesa na wasaka ngawira.

Tunatarajia utekelezaji haraka iwezekanavyo ili kurejesha heshima ya mamlaka ya rais na imani ya watu wetu.



Source: Tanzania Daima Februari 17, 2008.

No comments: