The Chant of Savant

Wednesday 26 December 2007

Kikwete tupe zawadi ya mwaka, vunja Baraza la Mawaziri




DESEMBA 21, vyombo mbalimbali vya habari vilimkariri Rais Jakaya Kikwete akisema hana mpango wala ulazima wa kuvunja Baraza la Mawaziri.

Hii inasikitisha na kukatisha tamaa. Maana si siri wala uzushi kwamba Baraza la Mawaziri la Kikwete licha ya kuwa zigo kubwa, limeshindwa vibaya kiasi cha kumfedhehesha na kumuangusha Kikwete ingawa hataki kukubali na kufanyia kazi ukweli huu kwa sababu anazozijua mwenyewe.

Kulikuwa na tetesi kuwa rais angevunja baraza lake la mawaziri na kuwatimua mawaziri wote wenye kuandamwa na kashfa za ufisadi.

Ingawa rais alijitoa kimasomaso na kuukana ukweli huu, alikiri kuwa baraza lake la mawaziri ni kubwa, hivyo ni mzigo na ni ukweli kwa wale tunaoshinikiza alivunje na kuunda jipya dogo na lenye watu safi tayari kuikwamua nchi hii iliyozamishwa kwenye uchafu wa ajabu utokanao na ufisadi, kulindana, kujuana na kuupuzia umma.

Pili, ieleweke kuwa uvumi huu unaokatwa ngebe na rais ni ishara na taarifa kuwa umma sasa unayasikia maumivu ya zigo hili alilotubebesha rais kwa sababu zake binafsi. Hii ni ishara ya kuasi na kusema ‘enough is enough’ ingawa watawala hawataki kuelewa hivyo.

Mlipa kodi anatweta na mizigo isiyo na ulazima, hasa kipindi hiki tunaposhuhudia kuporomoka kwa uchumi wetu na kutapanywa kwa fedha na rasilimali zetu kama taifa.

Tatu, kutamalaki kwa kashfa na vitendo vya kifisadi ukiachia mbali kushindwa kabisa kwa serikali, ni ishara kuwa rais naye kwa zamu yake na namna yake ameridhika na anguko hili la kihistoria kwa nchi yetu na kwa rais aliyeingia madarakani kwa ridhaa kubwa ya wananchi.

Nne, kuendeleza kebehi na kichwa ngumu kwa watawala ilhali alama za nyakati zinataka vinginevyo. Hivi rais ananufaika na nini kwa kuwa na utitiri wa mawaziri wasio na kazi ya kufanya bali kutapanya pesa ya umma na kutumia muda wa umma kwenye shughuli zao binafsi?

Je, hapa rais haoni kuwa adui wake ni yeye mwenyewe? Nani anamshauri vibaya rais kiasi hiki cha kugeuka kipofu dhidi ya ukweli ulio wazi?

Inashangaza kwa rais na waliomzunguka kuendelea kujiridhisha na baraza bomu kama hili. Hii inafanya swali, rais ananufaika vipi kuzidi kuchomoza kwa ukali wa ajabu.

Inawezekana rais hahisi mzigo huu wala maumivu yake! Je, ni kwa vile halipi kodi bali kuitumia na wenzake watakavyo? Atauhisije iwapo ameshindwa hata kusikiliza na kuvifanyia kazi vilio vya umma unaozidi kuteseka ilhali watu wachache wakizidi kuneemeka mgongoni mwake?

Au ni ile kudanganywa na kupumbazwa na wapambe wanaomtumia kutimiza ajenda zao za siri? Je, rais ameamua kusikiliza urongo wa wapambe wanaomuaminisha mambo ni safi wakati siyo? Ni hatari kiasi gani?

Je, msimamo kama huu ni busara au maangamizi ya baadaye kwake na nchi kwa ujumla? Kwanini rais hataki kuwasikiliza umma uliokata tamaa na kuelemewa na maisha magumu?

Kwa mtu anayejua siasa na utete wake, angedhani kuwa matokeo ya hivi karibuni ya REDET juu ya kuporomoka kwa imani ya umma, kwake yangekuwa onyo na andalizi la kubadilika na kuusikiliza na kuutumikia umma badala ya kuupuzia na kuutumia.

Kimsingi anayeumia ni mlipa kodi maskini. Kuna haja ya kumsadia rais. Baraza lake kubwa la mawaziri ni zigo zito hata kama kwake linaonekana jepesi kwa vile haligusi maslahi yake binafsi.

Hivi kweli kule vijijini - kwa mfano - unapoambiwa kuwa mwalimu mmoja anafundisha zaidi ya watoto 280 kama ilivyoripotiwa hivi karibuni na vyombo vya habari, wanamuelewa rais kweli?

Je, kwa kuwa na msimamo huu ulio hasi na hatari kwa wananchi, rais atashindwa kuonekana naye ni sehemu ya mzigo na tatizo? Je, hali hii inamjengea au kumbomolea rais?

Je, rais hata wasaidizi wake hawasomi magazeti na kuzidurusu taarifa kama hizo hapo juu ambapo ukweli dhahiri ni kwamba serikali yake imefeli vibaya? Kama hawasomi, ni kwanini kila asubuhi pesa ya mlipa kodi inafujwa kwenye kununua magazeti karibu yote ya kila siku ilhali hayatumiki wala kufanyiwa kazi?

Inashangaza na kutia wasi wasi kuona rais anaridhika na Baraza la Mawaziri ambapo wengi wao wanakabiliwa na shutuma za wazi kuhusiana na ufisadi uliotamalaki.

Je, rais yupo kwa ajili ya nani kati ya wananchi wanaoumia na wezi wachache wanaowaumiza wananchi? Kuna haja ya kupewa ukweli ili angalau umma ujue nini ni nini ili tuache kuonekana kama walalamishi na wazushi?

Tungependa hili liwe wazi ili tusionekane kama tunamuona rais kama mtu asiyekwenda na wakati.

Hili litatuepushia kuonekana kama wachochezi na wataka shari ingawa kimsingi wachochezi na wataka shari ni wale wanaomdanganya rais kiasi cha kumgeuza kama kijiko cha kuchotea utajiri utokanao na utumizi mbaya wa madaraka.

Watanzania wengi walidhani kuwa muda waliokuwa wamempa rais hata kudiriki kumtetea kuwa anaangushwa na watu wake, angeutumia vizuri kurekebisha hali ya mambo.

Je, kwa kuridhika na baraza lake la mawaziri haoni kuwa anawageuza wananchi wambea na majuha wasiojua wanachosema hata vipofu wasioona hali inavyozidi kuwa mbaya? Je, hili linamsaidia rais hata hao wapambe wake iwapo umma utaamua kuasi kama unavyoanza kuonyesha?

Inatia shaka sana kuona rais anaridhika na Baraza la Mawaziri lenye zaidi ya mawaziri nusu wanaokabiliwa na tuhuma za ufisadi ambazo wameshindwa kuzikanusha ukiachia mbali kutishia kwenda mahakamani na wasifanye hivyo.

Ziko wapi kesi za kudai kuchafuliwa majina tulizowasikia akina Nazir Karamagi, Grey Mgonja na wengine wakitishia kuzifungua?

Je, serikali yake ni ya nani kati ya watu wake na wananchi? Ni vizuri kuelezwa tuelewe ili tujue la kufanya. Na rais asipotoa jibu umma utajitafutia jibu kwa amani.

Huwezi kuwaambia wananchi kuwa serikali ni yao, na kisha hapo hapo ukawapuuzia kana kwamba hawajui wanachofanya wala wanachotaka!

Tumpe mifano hai. Kwa tuhuma zilizoelekezwa kwa baadhi ya viongozi, umma ulitegemea rais awawajibishe ili wachunguzwe vizuri.

Kwa yaliyotokea Muhimbili ambako maisha ya mwananchi asiye na hatia yameishapotea, wananchi walitegemea Waziri wa Afya awajibike mara moja badala ya kuwa ndiye kinara kwa kuunda tume ya kujichunguza.

Kwa yanayoendelea kwenye wizara za Elimu ya Juu; Miundombinu; Kilimo; Nishati na Madini, wananchi walitegemea rais awatimue wahusika ili kuwachunguza hata kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria ili haki itendeke na mali na rasilimali vya umma vinusurike. Lakini wapi! Je, rais tumueleweje?

Kuna haja ya wananchi kuachana na kutafuta majibu toka serikalini. Maana serikali sasa inaonyesha wazi kuwa haina majibu na kama inayo ama si sahihi au haitaki hata kuyatoa kwa sababu izijuazo yenyewe. Hii maana yake ni taarifa kuwa wananchi ni kama mayatima wasio na serikali.

Kuwa na serikali siyo kuwa na watu maofisini bali kuwa na huduma na heshima kama wenye nchi badala ya watu fulani kuiteka na kuitumia nchi na rasilimali zake watakavyo.

Pia kuna haja ya umma kukengeuka na kuacha kuwaachia upinzani kila kitu linapokuja suala zima la kuibana serikali ili itende haki ambayo kimsingi si ombi wala hisani bali wajibu.

Kwanini mwananchi alipe kodi na asipewe haki yake ya huduma na maamuzi juu ya uendeshaji wa serikali na nchi yake?

Rais vunja Baraza la Mawaziri hata kama kufanya hivyo ni kulazimika. Hali ni mbaya.

nkwazigatsha@yahoo.com


Source: Gazeti la Tanzania Daima Desemba 26,2007

No comments: