The Chant of Savant

Wednesday 21 November 2007

Kijiwe kilipounda kamati kuchunguza mikataba

Mpayukaji Msemahovyo
MKUU amekuja na sanaa mpya ya kujipiga mitama. Haoni aibu wala kustuka kwamba anaweza kustukiwa. Kama wana Kaya wameshindwa kustuka, Kijiwe kimestuka, tena ile mbaya.
Kimekutana kuunda kamati za kuchunguza Richmonduli na mikataba yote ya madini, mabenki, viwanda na uchukuaji kwa ujumla.
Leo Mpemba ni mwenyekiti wa kikao hiki nyeti.
Kikao kinaanza kwa Mpemba kukifungua rasmi.
Anatuguna mic. "Yakhe assalamaleko." Tunaitikia: waleko salama.
Anaendelea kukikandamiza. "Yakhe tusipoteze wakati tuanze kikao hichi mahsusi kuunda kamati za kuchunguza ulaaji."
Mikono ipo karibu yote angani. Mkurupukaji anapewa mic. Anaanza. "Wazee tusipige pembeni." Inasikika miguno. Yeye hajali anaendelea. "Mnashindwa kugunia wezi wenu mnagunia kupiga pembeni! Okey. Napendekeza baada ya kumaliza kuunda kamati za uchunguzi tuandamane kushinikiza kamati za mkuu zisimamishwe kwanza watuhumiwa wawajibishwe."
Huwa hatuna tabia ya kupiga makofi kama vyura wa Idodomya. Ila kwa alivyotukuna tunajikuta tukiangusha makofi.
Anaendelea. "Tuache utani. Tukiendelea kulialia ipo siku wajukuu zetu wata… hata kuchapa viboko makaburi yetu. Naomba kutoa hoja."
Mpemba anaangalia nani amlambishe mic. Anamteua mgosi Machungi.
Anakwanyua mic. "Wagoshi tikubaliane tena siiyansiii (seriously) kuanzisha haakati za ukombozi. Sijawahi kuona mtuhumiwa akijiundia tume ya kumchunguza! Hii ni kutiibia pesa yetu.
“Kwanza nani atawaamini wanakijiwe wa CCM? Huyu tikubaiane atakuwa mwehu. Hatiwezi kuchunguza watu kwa usaama wakiwa maofisini na vyeo wakilipwa pesa yetu. No imposhible kabisa."
Mbwa Mwitu wala hangoji mwenyekiti kumruhusu, anachumpa na kupora mic. "Kwanza tujulishwe ni kwanini kwa mfano Mkuu wa kijiwe bungeni na Mama Iron Lady waliudanganya umma, tena bungeni. Je, huu siyo ushahidi wa kimazingira unaoweza kutuonyesha akina Richmonduli ni nani? Wanadhani hatuwajui? Muda wa kufichana, kulindana, kuvumiliana na kugeuza majuha umekwisha. Enough is enough."
Kabla ya kuendelea, mzee Maneno anaonyesha alama ya time out. Mpemba anamzuia Mbwa Mwitu kuendelea, na kumruhusu mzee Maneno.
Anasema. "Yakhe Mbwa Mwitu simama nzee Maneno ana hoja ya kukuingilia."
Mbwa. "Ami tuheshimiane"
Mzee Maneno anatoa udhuru. "Wazee Kingereza kinazidi sana. Punguza hapa siyo Uingereza wala msijifanye kama wanakijiwe wa Idodomya wanaochanganya Kiswanglishi kuficha ukitaahira wao."
Baada ya kumaliza, Kapende anautuma mkono na kuruhusiwa. Anadanda. "Wazee hivi nani anaweza kumuamini Chekacheka? Yaani huu mwaka wa tatu anatudanganya kila siku. Sasa tukatae. Kama tume basi itumike tume yetu tusio na ufungamano na mshikamano na Li-siri-kali hili la urafiki na uanachama."
Mzee Mdomo anadandia mic. "Mzee mzima umepatia. Huwezi kumsafisha mtu kinyesi akiwa anaendelea kukikalia. Hatuwezi. Mkataba wa Guest House na Buzwagiro umetufumbua macho kuwa hawa watu wanatuona majuha na hawaaminiki. Jamaa alitwambia bila hata kuombwa angerekebisha mikataba na juzi juzi alisema kazi hii inakaribia kuisha. Sasa hii inayochunguzwa ni ipi?"
Mgosi anadandia. "Hata Ichimondi tiliambiwa na Takuu hakuna uchafu. Mbona sasa inaetwa ile ile au ni kutaka kutiibia kwa kujiipa njuuku zetu? Tikatae na tiandamane siyo tiishie kulia na kulaamika."
Makengeza naye hajivungi. "Turiwambia mkaona kama tunawadanganya. Hii iwe mala ya mwisho kunyamazia haya mazingaombwe.
“Mkuu mbona naye ana zigo lake kwenye list of shame. Akina Silaha wamegundua kuwa aliingia kwa rushwa tena kwa kuiba pesa yetu benki. Angekanusha au kuchunguzwa kwa hili badala ya kumwachia mbwa aunde tume ya kuchunguza aliyeiba nyama."
Mchunguliaji anadandia. "Mzee umenifikisha hapo. Tume imeundwa na mbweha, mbwa mwitu, vicheche, fisi na kondoo mmoja kabwela. Atawaweza wala nyama hawa wakati yeye ni mla majani?"
Mzee nadandia. "Huenda anataka kujifunza kula nyama aonje raha yake. Ila mwisho wa yote wataliwa watoto wake."
Msomi anaamua kutia timu baada ya kuona utaratibu wa mwenyekiti unadharauliwa.
Anaanza. "Wazee, maneno yenu ni mazito na ya kisomi kuliko wafata mkumbo wa Idodomya."
Kabla ya kuendelea Mbwa anaingilia. "Sisi ni wasomi kuliko wao maana hatuiuzi kaya yetu na watu wake, wakiwamo mama zetu kama wao."
Msomi anaendelea. "Uko sahihi. Mtu anaposaini mkataba wa miaka kwa kuangalia tumbo lake, anawatwisha mzigo wajao baada ya sisi kupita.
“Huyu ni muuaji wa waliopo, waliopita na wajao. Hii ni aina mpya ya ukoloni tena mchafu kuliko ule wa Mwingereza, Mreno na Mfaransa."
Kabla ya kuendelea simu inaita. "Yap. That’s pretty right. These guys are goofing thinking we too will keep on goofing and fluffing likewise."
Aliongea ung’eng’e mgumu kwa muda mrefu halafu akamaliza na kuendelea na mhadhara.
"Jamaa yangu wa chuo kikuu alikuwa akinieleza wasomi wanavyopanga kulaani kamati hii."
Kabla ya kuendelea Mzee Maneno anadakia. "Unaona. Kweli sisi ni wasomi hata kama hatukufika sokondari na chuo cha Manzese."
Msomi akiwa anatabasamu anaendelea. "Ni kweli mzee wangu. Usomi wa kuibia umma siyo usomi bali ujambazi unaoitwa usomi. Huu siyo usomi ni usumu. Tukirejea kwenye upuuzi huu, je Chekacheka ana udhu wa kutosha kuunda kamati adilifu? Ni nani anaweza kuukata mkono unaomlisha.
“Mbona juzi juzi mwenzao tena wakiwa kijiweni aliwapa kavu kavu kuwa wote wameingia mle kwa rushwa isipokuwa yeye ingawa alikosea kusema na Lwasha."
Anakatua shata lake na kupiga tama mbili tatu za tangawizi na kujikakamua na kuendelea.
"Huwa najiuliza mantiki ya kutoa tenda kubwa tena ya nchi kwa kampuni ya mfukoni kama Richmonduli! Je, hapa tunayemsaka ni yule yule anayejifanya kusimamia msako?
“Watazungusha na mizengwe siku moja wataumbuka. Viumbe hawa ni wagumu kujifunza. Yaani anavyohangaika na kuaibika Ben Tunituni Makapi halijawa somo tosha! Siku zilizopita mlimsikia mkuu wa kijiweni bungeni akikiri kuwa alikurupuka. Anangoja nini ofisini? Kiongozi anayekurupuka hafai hata kuingia ofisi ya umma. Alikurupuka ili iweje?"
Mbwa anajibu. "Hujui mshiko unakurupusha. Huoni madereva wa daladala wanavyokurupuka usiku na kukimbiza magari kama wanakwenda kujinyonga ili kupata pesa?"
"Kwa maana nyingine unamaanisha kukurupuka ni fumbo la imani, Kristo alikufa, Kristo alifufuka?"
"Kumbe sasa," anachomekea mzee Maneno.
Tuliunda kamati chini ya wenyekiti wa Mpayukaji Katibu Msomi na wajumbe wote.
Tukiwa tunajiandaa kuendelea kutoa hadidu za rejea, wapiga debe walianzisha ugomvi wa kugombea nauli, tukatimua mbio.
mpayukaji@yahoo.com www.mpayukaji.blogspot.com

No comments: