The Chant of Savant

Wednesday 14 November 2007

Falsafa na vijembe

Wajumbe wa CCM wamestuka
Mpayukaji Msemahovyo


KIJIWE kina furaha. Kwanza ni kwa kushinda gilba na hila kwa kutumia bomu liitwalo kuzomea.

Pili ni kwa kutupwa vimbelembele wa nambari wahedi akina Kingungo Ngumburu Mweupe na Tambo Hizo na wengine, hasa wachongaji peni waliojitia uana uongo siasia.

Tumekutana kwa heshima bila kufanya vituko na aibu kama kule Idodomya.

Baada ya kuzima fegi yake, Machungi analianzisha. “Wagosi tijipongeze timeshinda. Timezomea. Timenyanyasa na timetoa taaifa kuwa tinaweza hata bia Kikwekwe na watu wake.”

Mkurupuki anaweka kahawa yake mezani na kudandia mic. “Tilionya waache kimbelembele hawakusikia.” Kabla ya kuendelea, Mgosi anaonekana kuchukia kuigizwa huku kijiwe kikiwa hakina mbavu.

Anaendelea. “Hawa vidhabu hawakujua hata wezi wenzio wamewastukia kwa kupiga domo kaya! Sijui waliboa, anajisikiaje kujitoa udhu kutetea uoza.”

“Wanasiasa wetu hawakujaliwa aibu. Hukumsikia Mgosi akiwapa I love you utadhani anawa-love kweli? Hakuna waliponikuna kama kuwatupa hawa vidhabu.” Anachomekea Kapende huku akiweka vizuri kamera yake utadhani anataka kutoa picha ya upuuzi wa Idodomya.

Mzee Maneno anachumpa na kulamba mic. “Nyinyi hamjui. Ulaji unalevya kiasi watu hujisahau na kujishaua wasijue wote ni vibaka wanaoviziana. Kwa Mkuu huyu Cheka Cheka na wapambe uchwara wake wenye roho mbaya ulitegemea nini? Hata babu mwenzangu Msukwa akae akijua.”

Mpemba naye anatia buti. “Yakhe mie tangu wamgeuke Kamandoo sina hamu na wanasiasa Wallahi. Wasema uchumi unkua wakati wafa!”

Makengeza analamba mic bila kungoja. “Jamaa yangu wa Uhasama wa Taifa amenitonya kuwa mtandao unaanza kuwaengua wanaoonekana kuwa mizigo na wajanja ili ujichimbie. Cheka Cheka kazidiwa. Anataka watu wanaoweza kujituma na kulinda sanaa zake. Huoni Chwenge anayesifika kwa kutuingiza mkenge kwenye mikataba mingi alivyosogezwa karibu? Wajameni chama hicho kinaporwa na mbweha toka kwa makabwela.

“Hata hii ya kujifanya wamentosa Azoza ni gea tu. Nimenyunyuziwa nyuzi atakuwa waziri wa viwanda avimalizie vyote!”

Mchunguliaji anaingilia. “Mzee nakupongeza.” Ananiangalia akitabasamu na kuendelea. “Nakushukuru. Kimbelembele wa Cheka Cheka na Bw. Mdogo hawakugombea. Ni baada ya kuwapaka. Si unajua Bi. Mkubwa anavyopenda ukuu bila kuchaguliwa?”

Akiwa anajiandaa kuendelea kumsiliba Bi. Mkubwa, Mpemba alidaka mic na kutafuna. “Yakhe mie hakuna aliponkuna kama kutomteua Sumaiye au Luwasha. Hawa hawana kitu yakhe. Mie nahisi hii ni kutafuta nanna ya kujisafisha hasa genge lake.”

Mpayukaji sijivungi, natia guu. “Nyuzi nilizo nazo ni kwamba baraza la maulaji litavunjwa na mashoga zake watapigwa chini kuanzia juu hadi chini. Jamaa amezidiwa na anaonekana kuwa tayari kuwatosa maswahiba zake.”

Nikiwa najiandaa kujimwaga vilivyo si Mbwa Mwitu alidakia. “Japo wanasiasa wetu hawaaminiki, je jamaa anao ubavu hata kama amelemewa?”

Mzee nimepata upenyo namchomekea. “Intelijensia yangu inanitonya kuwa wafuatao watatimuliwa. Nakamuaa kombe langu na kuendelea kujinoma huku kijiwe kikiwa kimetulia na kunipa yote mawili na nyongeza ya mimacho.

Naanza kwa manjonjo. “Mkuu atatanua ifuatavyo. Sasa panga linaangukia watu. Atasema Luwasha nje. Sababu? Una rekodi mbaya hata utendaji wako ni wa kiujanja ujanja na isitoshe umetajwa na Dk. Silaha. Pia safari zako nyingi huwa sizielewi elewi.”

Naendelea. “Atakohoa kidogo na kucheka cheka kama kawa na kuendelea. Kadamagi N out, wewe uliniletea balaa na rafiki yako kwa kunizunguka na kusaini Buzwagio.”

Atamkazia macho huku Kadamagi akiinama kwa aibu na mshangao kuona ametoswa haraka kama ilivyotokea kwa Machelani. Ataendelea. “Ndugu zangu, eleweni kuongoza nchi siyo sawa na kampuni zenu. Tamaa za baadhi ya watu zimefanya Kaya isikalike wala kutawaliwa. Kwa tamaa hizi hizi tumewapoteza hata wenzetu wasio na hatia.”

Atakohoa na kufikicha vidole na kuendelea. “Wengine tutakaolazimisha kutokuwa nao ni Miramba BP, Mangai J na Wasiri S. Nyinyi ni vibabu na hamna jipya wala kasi mpya, Chwenge A, wewe ushauri wako mfu umemponza rafiki yangu Tunituni, Membo, Kupuya JA, mmesoma lakini hamna mpya pia, Kingungo NM na Marumaru P, hawa wawili ni kwa sababu ya kupayuka ovyo ovyo.”

Atacheka kidogo na kuangalia huku na huko ili kula ujiko na kuendelea. Msolowa P out. Wewe ulivurunda SUA na kwenye mikebe ya ilmu ya juu. Wengine…”

Wakati najiandaa kuendelea kuwatonya, alipita Tambo Hizo tukaanza kumzomea. Baada ya kumaliza, tuliendelea na stori ya kutupwa kwa waliokuwa wakijiona kama mioyo ya Chama Cha Mapinuzi Mpinduzi.

Mzee Maneno anakula mic. “Jamani hebu wenzangu nisaidieni. Hivi kweli hiki chama kinaweza kurejea hadhi yake ya wakati wa mzee Mchonga?”

Msomi anatia timu bila kungoja wala kutoa taarifa. “Wazee huku ni kutapatapa kwa mfa maji. Kitanusurika vipi iwapo kwanza hakina dira. Na pili kimebinafsishwa kwa wenye nazo?” Anainua kikombe chake cha tangawizi maana tangu arejee toka kuzomea inaonekana si haba amekatiwa kidogo. Hata kisimu amebadilisha ana iPod.

Anaendelea. “Sisi tunaangalia mageuzi mkorogo kwenye chama. Wanakaya wameishaamka na wako tayari kwa lolote. Ndiyo maana nashawishika na maneno ya Mzee Mwenyewe.” Anageuka na kuniangalia akitabasamu na kuendelea.

“Jamaa kweli kazidiwa na anatapatapa. Anatafuta njia ya kujitoa kwenye tope alimozamishwa na maswahiba zake wapenda pesa. Maskini wamemteka na kumpumbaza kiasi cha kuwa kama hana masikio, macho wala ubongo!

Bila kufa na mtu hasa hawa mafisadi, atajikuta akianguka mweleka wa mende. Jamani wanakaya licha ya kuwa na hali mbaya huko madongo poromoka, wana hasira naye. Mapenzi yamegeuka kuwa chuki na zile tambo za ‘ni kipenzi cha watu’ zimegeuka ghafla kuwa adui wa umma!”

Anakatua andazi na kunywa tangawizi kidogo huku akisogeza ki-iPod chake na kuendelea. “Mie nilikuwa Serengeti, Utegi, Mugumu hadi Sirari. Hadi yule jamaa aliyetungua helikopta kwa manati nimeonyeshwa na jamaa wanamheshimu na kumuona mkombozi. Jamaa asipofanya kweli akawatema mafisi waliomzunguka ndiyo asahau ukuu kabisa.”

Anageuka kumkaripia Mbwa Mwitu anayevuta sigara yake ya Kali. “Mbwa, jamani hizo bange zenu zinatuumiza.” Mbwa anazima kisigara chake na Msomi anaendelea kutuguna mic.

“Nijuacho ni kwamba jibu la matatizo ya kaya hii ni kusuka upya kikosi cha mashambulizi. Akiendelea na uswahiba jamaa atajikuta pabaya na kaya inaweza kuingia machafuko. Watu wanawajua mafisadi kama viganja vyao!”

Tukiwa tunajiandaa kuendelea, rafiki yake Msomi alikuja na ripoti ya BoT.

Msomi anaanza kuiponda. “Who pays the piper picks the tune.” Hakufafanua.

Msomi akiwa anajiandaa kutusomea, kunguru aliunganisha nyaya za umeme na kutokea shoti na mlio mkubwa. Nilitimka haraka kuokoa nafsi yangu.

E-mail: mpayukaji@yahoo.com
Blog: mpayukaji.blogspot.com

No comments: